MKUU WA WILAYA YA CHEMBA AFANYA ZIARA KATIKA TARAFA YA
FARKWA NA KWAMTORO.
Mkuu wa Wilaya ya
Chemba Ndugu Simon Odunga alifanya ziara katika Tarafa ya Farkwa na Kwamtoro kuanzia
tarehe 19-20/8/2016 akiambatana na Kamati ya ulinzi na Usalama ya Wilaya na baadhi
ya watendaji wa Halmashauri.
Katika ziara hiyo
alifanya mikutano ya hadhara na wananchi wa vijiji vya Tumbakose, Farkwa,
Bubutole, Gonga, Kwamtoro, Magungu na Sanzawa. Alizungumza na wananchi kuhusu masuala
ya Elimu, Maji, Afya, Ulinzi na Usalama, Chakula, Ardhi, na kusikiliza kero na
changamoto za wananchi wa maeneo hayo.
Katika kijiji cha
Tumbakose wananchi walikuwa wanavutana juu ya ujenzi wa ofisi za kata katika
kijiji cha Tumbakose au Humekwa. Mkuu wa Wilaya aliwashirikisha wananchi kwa
kuwaomba waseme ni kijiji gani wanataka kiwe kata.Wananchi walisema kijiji cha Tumbakose ndiyo maamuzi yao ya
kwanza kuwa kata na waliamua wakiwa katika kata mama ya Gwandi kabla ya
kugawanywa. Kutokana na uamuzi huo, Mkuu wa wilaya alitoa agizo kwa viongozi wa
vijiji vya Humekwa, Hawelo na Tumbakose kuanza ujenzi mara moja ya ofisi za
kata katika kijiji cha Tumbakose.
Mkuu wa Wilaya
akiwa katika Mikutano ya hadhara alikemea tabia ya wanaume kufanya mapenzi na
wanafunzi wa shule kwani ni kosa la jinai. Alitoa agizo kwa vyombo vya dola
kuwakamata wale wote wanaojihusisha na tabia hiyo mbaya ili sheria iweze kuchukue
mkondo wake. Alisema kuna tabia ya wazazi wa wanafunzi wanaopewa mimba na
wahalifu kurubuniwa kwa kupewa fedha ili wazazi hao wasiende kutoa ushahidi mahakamani.
Alisisitiza wazazi wanao fanya hivyo waache mara moja kwani nao ni wahalifu
watakamatwa na kufikishwa mahakani. Pia alipata fursa ya kuwasilimia wanafunzi
wa sekondari ya Farkwa na kuwasihi kusoma kwa bidii kwani elimu ndiyo dira ya
maisha na waepuke migomo ambayo mwisho wako ni kufukuzwa shule. Aliwahidi
wanafunzi kuwa serikali ya wilaya itanunua pampu mpya ya maji na kuifunga wiki
ijayo ili kuondoa tatizo la maji wanalopata kwa sasa.
Mkuu wa wilaya aliagiza vijiji vyote vya
wilaya ya Chemba kuunda kamati za maji za vijiji pia vikishirikisha wanawake
kama Sera ya maji inavyoagiza. Kamati hizi zitaratibu uendeshaji wa maji katika
vijiji vyao na fedha inayopatikana itatumika kuboresha matandao wa maji hapo
kijijini kwa kununua vifaa.
Mkuu wa wilaya
aliagiza ifikapo mwezi wa 10/2016 kila kaya katika vijiji vyote vya wilaya ya Chemba
kuwa na choo na pia kujiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF). Aliwataka
watendaji wa vijiji na kata kusimamia zoezi hilo kwani baada ya muda huo kupita
atafanya ziara ya kukagua kama wametekeleza. Amesisitiza gharama za kulipia
mfuko wa afya ya jamii kwa watu sita katika kaya ni Tsh.13,000/= na watapata
huduma ya afya katika zahanati, kituo cha afya na hospitali bila kutoa gharama
yeyote tena kwa mwaka mzima. Aliongeza kwa kusema wazee wote wenye umri wa
kuanzia miaka 60 na kuendelea hasa wasiojiweza wanatakiwa kupatiwa vitambulisho
ili watibiwe bure kama ilivyo kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 5. Alitoa
onyo kwa wahudumu wa afya walio na tabia ya kutotoa huduma kwa haraka kwa
wanachama wa mfuko wa CHF na kupendelea wanao toa fedha mkononi waache tabia
hiyo mara moja kwani sheria za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni
pamoja na kusimamishwa kazi ili wakafanye kazi zingine wanazoona zinafaa kuliko
kuwanyanyasa wananchi.
Mkuu wa wilaya
alisema, kuna baadhi ya wananchi, viongozi wa vijiji na kata wanawakaribisha
wahamiaji katika vijiji vyao na kusababisha migogoro ya ardhi. Kuanzia tarehe
06/8/2016 amesimamisha uuzwaji wa ardhi na ukaribishaji wa wahamiaji katika wilaya
ya Chemba hadi hapo atakapo toa maelekezo mengine. Ameagiza viongozi wote wa
vijiji, kata, tarafa na wilaya kusimamia zoezi la kupanga matumizi sahihi ya
ardhi kwa kutenga maeneo ya wafugaji na wakulima ili kuepuka migogoro ya
wakulima na wafugaji.
Pia alionya wale
wote wanao leta choko choko za uvunjifu wa amani kwa kusema watashiriki
maandamano ya UKUTA yanayoandaliwa na chama cha chadema kuanzia tarehe 01/9/2016
wasithubutu kufanya hivo kwani watakabiliana na vyombo vya dola na hawataonewa
huruma kwa sababu ni wavunjaji wa amani katika nchi yetu. Vilevile aliwasihi
wananchi kuuheshimu Mwenge wa Uhuru kwasababu ni alama ya Uhuru wetu tuliopta
mwaka 1961 ambapo mwasisi wa taifa letu Mwalimu J.K.Nyerere alipigania wakati
anadai Uhuru na kuupandisha kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro. Akasisitiza
kuwa bendera ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina alama ya Mwenge wa
Uhuru, majeshi ya ulinzi na usalama kwenye kofia zao zina alama ya Mwenge wa
Uhuru pia.
Kwa upande
mwingine, Mkuu wa wilaya amesema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dr. John Pombe Magufuli haitatoa chakula
bure kwa mwananchi yeyote asiyefanya kazi. Amesisitiza kwa kusema chakula kitatolewa kwa mwananchi ambaye
amefanya kazi lakini kutokana na sababu za kidharura hakuweza kupata chakula kwa
mfano, amelima lakini kutokana na ukame hakuweza kuvuna, amelima lakini wakati
wa mavuno chakula kikaharibika kutokana na mvua kubwa kunyesha kama ilivyotokea
kwa baadhi ya wananchi wa wilaya ya chemba kupata ugonjwa wa SUMUKUVU lakini
serikali imewapatia chakuala bure.
Katika mikutano ya
hadhara Katibu tawala wa wilaya Ndugu Nyakia Ally aliwaambia wananchi kuwa
atatoa namba ya simu kwa watendaji wa vijijiji vyote vya wilaya ya Chemba ili
wawape wananchi namba hiyo lengo wawe wanatuma ujumbe wa meseji tu kuripoti kero
wanazokumbana nazo na ofisi ya Mkuu wa wilaya itakuwa inazishughulikia.
Zifuatazo ni
baadhi ya picha za mikutano ya hadhara ;
Mkuu wa wilaya ya Chemba Ndugu Simon Odunga akiongea na wanafunzi wa Farkwa Sekondari.
Mkuu wa wilaya ya Chemba Ndugu Simon Odunga akiongea na wananchi wa kijiji cha Bubutole kata ya Farkwa.
Katibu Tawala wa wilaya ya Chemba Ndugu Nyakia Ally akiongea na wananchi wa kijiji cha Magungu kata ya Mpendo.
Mkuu wa wilaya ya Chemba Ndugu Simon Odunga akiongea na wananchi wa kijiji cha Kwamtoro.
No comments:
Post a Comment