Monday, September 5, 2016

TAARIFA ZA IDARA/VITENGO KATIKA MAENEO YA UWEKEZAJI, MAFANIKIO NA CHANGAMOTO.

IDARA YA ELIMU SEKONDARI.
UTANGULIZI.
Idara ya elimu sekondari imejikita zaidi kwenye taaluma katika shule za sekondari na kutoa taarifa mbalimbali zinazohusu vyuo vilivyopo ndani ya Halmashauri. Idara inasimamia shule za sekondari 22 za serikali na 01 ya binafsi.  Kati ya shule hizi 23 kuna shule tatu (03) za kidato cha tano ambazo ni Farkwa Sekondari, Msakwalo Sekondari na soya Sekondari. Katika ngazi ya vyuo, idara haina chuo chochote inayosimamia katika halmashauri yetu.

MAFANIKIO YA IDARA KWA MIAKA MITATU.
Kwa kipindi cha miaka mitatu (2013/2014 hadi 2016/2017) idara imefanikiwa katika shughuli zifuatazo:-
  • Kuanzisha shule za kidato cha tano. Kwa miaka mitatu sasa idara imefanikiwa kuanzisha shule tatu za kidato cha tano michepuo ya sayansi, sanaa na biashara. Shule hizo ni Farkwa sekondari mchepuo wa biashara kwa Tahasusi za HGE na EGM kwa wasichana, Msakwalo sekondari mchepuo wa Sanaa kwa Tahasusi za HGL na HGK kwa wavulana na Soya sekondari  Mchepuo wa sayansi Kwa Tahasusi za PCB na PCM wavulana. Halmashauri imefanikiwa kuwa na shule za sekondari za Serikali kwa kila Kata isipokuwa kata ya Jangalo na Paranga ambazo zina shule mbili kila moja. Shule zenye Daharia ni 03 tu ambazo ni Msakwalo, Farkwa na Makorongo. Kukosekana kwa Daharia (Hostel) kunawafanya wanafunzi watembee mwendo mrefu na kusababisha utoro kwa wanafunzi.
·         Kuongezeka ufaulu mitihani ya taifa kidato cha Pili, Nne na Sita. Kwa muda wa miaka mitatu ufaulu wa mitihani kidato cha pili umepanda kutoka 76% mwaka 2013, 82% mwaka 2014 na 96% mwaka 2015. Kwa Kidato cha Nne ufaulu umepanda kutoka 48.6%  mwaka 2013 hadi 56% mwaka  2014 . Kidato cha sita 2016 shule ya sekondari Msakwalo imefaulisha kwa asilimia 100% na ndio matokeo ya kwanza kidato cha sita katika Halmashauri yetu.

·   Ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya shule. Idara imefanikiwa kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo:
Ø  Ujenzi wa nyumba mbili (02) za walimu shule ya sekondari Lalta na Itolwa. Pia shule moja ya kukaa familia sita (six in one multiunit house) ambayo iko hatua ya umaliziaji katika shule ya sekondari Mpendo. 
Ø  Ujenzi wa  madarasa mawili (04) shule ya sekondari itolwa na Gwandi na Madarasa 04 shule ya sekondari Mpendo ambayo yako hatua ya umaliziaji
Ø  Ujenzi wa matundu ya vyoo vya wanafunzi 08 na 02 ya walimu shule ya sekondari Gwandi.
Ø  Ujenzi wa maabara 01 shule ya sekondari Goima na maabara zingine 61 zikiwa kwenye hatua mbalimbali za umaliziaji na lenta.
Ø  Ufungaji wa umeme jua kwa shule sita za sekondari ya Farkwa, Makorongo, Msakwalo, Kwamtoro, sanzawa na Mpendo.

CHANGAMOTO.
i.          Upungufu wa miundombinu na samani za shule ikiwa ni pamoja na nyumba za walimu, maabara, maji, umeme, vyoo pamoja na upungufu mkubwa wa viti na meza za wanafunzi pamoja na walimu.
ii.                  Ukosefu wa usafiri wa idara kwa ajili ya kufanya ufuatiliaji wa taaluma shuleni.
iii.                Ukosefu wa ofisi ya idara.
iv.                Upungufu wa rasilimali watu katika idara na shuleni pia.
v.                  Ufinyu wa bajeti ya uendeshaji wa ofisi na shule.

UWEKEZAJI.
Ujenzi wa shule ya sekondari ya bweni kidato cha I-VI. Lengo la uhitaji wa shule 01 ya sekondari katika makao makuu ya Chemba ni kuweza kuwa na shule 01 ya Bweni kidato cha kwanza hadi Sita iliyo kamilika katika Miundombinu yote. Fursa zinazoiwezesha shule hii ni pamoja na:
i)             Kuwepo kwa eneo lililopimwa tayari kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.
ii)            Makao makuu ya wilaya kutokuwa na shule ya sekondari kwani shule ya kata ipo umbali wa kilomita 10 toka makao makuu ya wilaya. Umbali huu unasababisha wanafunzi wa wakazi wa Chemba kutoifikia shule hiyo kwa urahisi.
iii)          Kuwa na shule 01 ya mfano ya bweni iliyokamilika kwa miundombinu kuanzia kidato cha Kwanza hadi cha Sita.

UMALIZIAJI WA UJENZI WA DAHARIA KWA KILA SHULE YA SEKONDARI.
Kati ya shule 22 za sekondari za Serikali wilaya ya Chemba ni shule 03 tu ndizo zenye Daharia (Hosteli) ambazo ni Msakwalo, Farkwa na Makorongo. Lengo la ujenzi wa Daharia kwa kila shule ya sekondari ni kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Jumla ya Daharia 38 zinatakiwa zijengwe kwa shule 19, kila shule inatakiwa na Daharia 02.
Lengo la ujenzi wa Daharia (Hostel) ni:
i)             Kuondoa utoro wa rejareja na wa kudumu kwa wanafunzi, hii ni kutokana na shule nyingi za sekondari kuwa mbali na maeneo wanakoishi jamii. Imebainika kwamba wanafunzi wanaotoka umbali wa kilomita 10 na zaidi wameonekana kuwa watoro shuleni.
ii)         Kuinua taaluma kwani wanafunzi wanapo kuwa wanaishi shuleni wanakuwa na muda mwingi wa kujisomea na kuondokana na shughuli za kijamii zinazoathiri ujifunzaji kwa wanafunzi.
iii)     Kupunguza tatizo la Wanafunzi wa kike kupata ujauzito.Imethibitika kwamba wanafunzi wa kike wanapata vishawishi wawapo uraiani kuliko shule za Bweni.
iv)        Kuinua taaluma kwani wanafunzi wanapo kuwa wanaishi shuleni wanakuwa na muda mwingi wa kujisomea na kuondokana na shughuli za kijamii zinazoathiri ujifunzaji kwa wanafunzi.
v)      Kupunguza tatizo la Wanafunzi wa kike kupata ujauzito.Imethibitika kwamba wanafunzi wa kike wanapata vishawishi wawapo uraiani kuliko shule za Bweni.

IDARA YA ARDHI NA MALIASILI.
 UWEKEZAJI.
Idara ya Ardhi na Maliasili imebainisha maeneo yafuatayo kwa ajili ya uwekezaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba.
i.             Uwekezaji wa viwanda vidogovidogo na vikubwa, shule za awali kwa ajili ya kuvutia wawakezaji mbali mbali na kusogeza huduma karibu na jamii.
ii.            Ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kupitia Shirika la nyumba la Taifa (NHC) ili kuweza kukidhi matakwa ya watumishi kwa kupata makazi katika makao makuu ya Wilaya ya Chemba. Pia maeneo ya sokoni, stendi ya mabasi, hospitali inatakiwa viwanja vyake kuendelezwa kwa haraka zaidi ili wananchi waweze kupata huduma muhimu.
iii.           Maeneo mengine ni benki, shule za Msingi na sekondari, vyuo, Ufugaji wa nyuki naTaasisi zingine zinazo jishughulisha na shughuli za maendeleo.

 MAFANIKIO.
Katika mwaka wa fedha 2015/2016 Idara ya Ardhi na Maliasili imefanikiwa katika mambo yafuatayo;

ARDHI.
Kupima viwanja vya matumizi mbalimbali vipatavyo 539 kitalu A na 596 kitalu D katika makao makuu ya Wilaya ya Chemba. Pia tulishapima viwanja 654 kitalu B na watu wanaendelea kujenga majengo yanayokidhi mahitaji ya ujenzi bora na wa kisasa.

 NYUKI.
i.             Kuwezesha Halmashauri kuwa na mpango mkakati wa kuendeleza ufugaji nyuki kiwilaya na sheria ndogo ndogo za Wilaya kuhusu kuendeleza raslimali ya nyuki.
ii.            Kwa kushirikiana na WVI Tanzania, Farkwa ADP Kuwezesha uanzishwaji wa manzuki ya mfano na mafunzo shule ya sekondari Farkwa yenye jumla ya mizinga ya kisasa 200.
MISITU.
i.             Kudhibiti uvunaji na usafirishaji haramu wa mazao ya misitu. Doria zilifanyika katika maeneo ya Kata za Kwamtoro na Farkwa, kuimarisha ukaguzi katika Mageti ya Babayu, Kinyamsindo, Mrijo, Kidoka na Tandala. Kazi hii imefanyika kwa ushirikiano na TFS.
ii.             Kuendelea na zoezi la usimamizi wa ukusanyaji wa mbao za madawati kwa ajili ya shule za Msingi na Sekondari, Kazi inaendelea na Mafanikio ni makubwa hadi sasa.

WANYAMAPORI.
Ufuatiliaji wa Taarifa za wanyamapori wakali na wakubwa , Kazi hii imefanyika kwa ushirikiano wa Pori la akiba Swagaswaga , Mkungunero na Polisi Chemba katika maeneo ya vijiji vya Tandala, Mtakuja, Igunga, Mialo na Kwamtoro.

CHANGAMOTO.
i.             Wananchi wenyeji hawabadiliki kutokana na mji unavyotakiwa kwa kujenga majengo bora, kuhamisha mifugo n.k.
ii.            Dhana ya kugawana viwanja halmashauri na wananchi imesababisha misuguano na wananchi wenye maeneo yao.
iii.           Kutokuwepo kwa fedha za kupima  maeneo yaliyobakia.
iv.           Matumizi ya madawa ya kilimo ambayo yanasababisha vifo vya nyuki.
v.            Uchomaji moto mapori ambao unaunguza miti muhimu kwa utoaji wa asali na mizinga.
vi.           Ufyekaji wa misitu unaofanywa na wakulima wakati wa kuandaa mashamba mapya ya kilimo.

MIKAKATI.
i.    Kuendelea na utoaji wa elimu kwa wananchi kwa kushirikiana na idara zenye ushawishi mkubwa kama vile maendeleo ya jamii.
ii.      Kuandika andiko la kuomba mkopo ili kulipa fidia na kupima maeneo ya block C, E, na F ili kuweza kudhibiti uendelezaji holela wa viwanja.
iii.    Kutoa elimu ya utunzaji wa Mazingira kwa wananchi ya kupanda miti kwenye maeneo yao pamoja na kulinda hifadhi ya milima  inayozunguka Wilaya ili  iweze kuwa na mandhari inayovutia na kuleta hewa safi kwa kushirikiana na Idara ya Mazingira.
iv.    Uwanzishwaji wa mashamba manne ya uendelezaji ufugaji nyuki kwa kushirikiana na Wakala wa huduma za Misitu Tanzania (Tanzania Forest Service (TFS).

 IDARA YA ELIMU MSINGI.
 UWEKEZAJI.
  1. Kuanzisha/kujenga shule ya ufundi (VETA) katika kijiji cha kambi ya nyasa.
  2. Kuanzisha/kujenga shule ya Kiingereza (Medium school darasa la Awali – Kidato cha nne) katika kijiji cha Kambi ya Nyasa.
  3. Kuanzisha/kujenga shule maalum ya watoto wasioona na viziwi (Darasa la Awali  - Darasa la saba.
MAFANIKIO.
i.        Kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu wa mtihani wa darasa la saba kutoka asilimia 30 hadi 47.
ii.      Waratibu Elimu Kata kuwezeshwa usafiri wa Pikipiki pamoja na rukuzu kwa ufadhili wa mpango wa Equip – Tanzania inayorahisisha ukaguzi wa shule kwa lengo la kuinua taaluma shuleni.
iii.    Kuongezeka kwa kiwango cha uandikishaji kwa kuanzishwa madarasa 70 ya utayari chini ya Mpango wa Equip – Tanzania.
iv.    Walimu Wakuu na Waratibu Elimu Kata kupata mafunzo ya uongozi chini ya mpango wa Equip – Tanzania.
v.      Walimu kupatiwa mafunzo kazini ambayo yamesaidia kupunguza idadi ya wanafunzi wasiojua KKK.
vi.    Kamati za shule zote 103 kujengewa uwezo wa kusimamia shule.

CHANGAMOTO.
i.      Ukosefu wa usafiri (gari la Idara ya elimu).
ii.    Upungufu mkubwa wa miundombinu na samani mfano madarasa na nyumba za walimu, meza, viti na kabati.
iii.   Kuwepo kwa miundo mbinu ya shule isiyokamilika mfano katika nyumba za walimu na madarasa.
iv.   Upungufu wa vitendea kazi kwa ajili ya mifumo ya taarifa kama vile internet, komputa, printa na mashine ya kudurufu.
v.    Maeneo ya shule kutopimwa na kukosa Hati miliki.
vi.   Uchakavu wa miundo mbinu ya shule.
vii.  Ukosefu wa vyumba maalum (Strong room) kwa ajili ya kuhifadhia mtihani.

IDARA YA KILIMO, UMWAGILIAJI NA USHIRIKA.
 UWEKEZAJI.
                                i.            Kujenga masoko ya mazao kwenye maeneo ya kata ambayo uzalishaji wa mazao ni mkubwa, mfano Mrijo, Soya, Kidoka, Jangalo n.k.
                              ii.            Kuanzisha/kujenga skimu za umwagiliaji katika maeneo yenye fursa hiyo(potential areas)
Mfano; Kidoka, Paranga na Jogolo.

CHANGAMOTO.
                                i.            Bei za mazao kubadilika mara kwa mara.
                              ii.            Upungufu wa raslimali watu.
                            iii.            Kutokuwa na usafiri.
                            iv.            Kutopata fedha za miradi kwa wakati.

MAFANIKIO.
                                i.  Tumeendelea kutoa huduma za ugani kwa kutumia mbinu mbalimbali mfano kuanzisha mashamba darasa,mashamba ya mfano n.k
                              ii.   Tumeendelea kusimamia miradi ya idara ya kilimo katika wilaya yetu, kwa mfano; miradi ya ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao na ujenzi wa mashine za kukamulia alizeti.

IDARA YA MAENDELEO YA JAMII.
 MAFANIKIO.
i.             Idara imeweza kuhamasisha uanzishaji na kusajili jumla ya vikundi 460 vya uzalishaji mali vya kiuchumi na kijamii.
ii.            Jumla ya kaya 85 zimepata mafunzo ya ujasiliamali, ufugaji nyuki wa kisasa pamoja na mradi wa ufugaji nyuki.
iii.           Idara imefanikiwa kuwezesha kaya masikini 5,344 kupitia mpango wa TASAF  III.
iv.           Tumefanikiwa kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa vikundi vya uzalishaji mali vya wanawake   12 na vya vijana 9.
v.            Tumefanikiwa kuwalipia ada na michango muhimu watoto 143 waishio katika mazingira hatarishi waliopo shule za sekondari na vyuo.
vi.           Idara imefanikiwa kuunda kamati za kusaidia watoto waishio katika mazingira hatarishi katika vijiji 10 kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la CCT pamoja TUWALEE.

    CHANGAMOTO.
i.             Ukosefu wa fedha za kutosha za kuwezesha vikundi vya wanawake na vijana.
ii.            Uhaba wa rasilimali watu katika idara.
iii.           Uhaba wa rasilimali fedha zinazotolewa ambazo ni ruzuku katoka serikali kuu.
iv.           Ukosefu wa vitendea kazi katika ofisi kama kompyuta na printa.

MATARAJIO YA IDARA.
i.              Kutoa mafunzo endelevu ya uingizwaji masuala ya jinsia katika mipango na bajeti ngazi zote.
ii.            Kuwa na mfuko endelevu wa utoaji wa elimu jinsia.
iii.           Kutoa elimu ya kuweka na kukopa kwa vikundi vya wanawake na vijana.

MFUKO WA AFYA YA JAMII (CHF).
UWEKEZAJI.
i.Kutafuta wadau mbalimbali kulipia kaya maskini kama; wafanyabiashara, viongozi mbalimbali ili kuongeza idadi ya kaya zisizojiweza kunufaika na huduma hii.
ii.Kuongeza uhamasishaji kwa kutumia mbinu mbalimbali.

CHANGAMOTO.
i.Upungufu wa watumishi wa afya katika sehemu za kutolea huduma.
ii.Watoa huduma wengi kutojua jinsi ya kuwasilisha madai.
iii.Kutokuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya kufanya uhamasishaji.

MAFANIKIO.
                                i.            Tumefanikiwa kuandikisha kaya 10,401 kati 39,285 kwa kaya lengwa kwa wilaya ya chemba,na kufikia asilimia 26.48% ya uandikishaji.
                              ii.            Tumefanikiwa kufanya uhamasishaji juu ya malengo, umhimu, mfumo na faida za CHF kwa maeneo mengi ya wilaya ya Chemba.

IDARA YA MAJI 

Hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Halmashauri ya wilaya ya Chemba ni kuwa wakazi wapatao 73,231 kati ya 235,711 wanapata huduma ya maji safi na salama sawa na asilimia 31 ya wakazi wote. Idara ya maji Wilaya ya Chemba inaendelea na jitihada za kutafuta vyanzo vingine vya maji ili wananchi ambao hawajafikiwa na huduma ya maji waweze kupata maji safi na salama ndani ya mita 400 kama sera ya maji ya mwaka 2002 inavyoelekeza.

UBORESHAJI WA HUDUMA YA MAJI.

Halmashauri ya Wilaya ya Chemba imekarabati  na  inaendelea na ukarabati  wa miradi ya maji yenye kuleta matokeo ya haraka (Quick wins) katika vijiji vya waida, Chase, sori na Lahoda/Kisande ambapo mchakato wake umefanyika na Halmashauri ya Wilaya ya Chemba.
Utekelezaji wa Miradi ya maji ni kama ifuatavyo;
i.             Ukarabati na usambazaji wa  maji katika kijiji cha waida umekamilika  ambapo wakazi wapatao  2,622 wananufaika na mradi huo, mradi huu umegharimu Tshs. 168,950,000.00 ambapo kazi za ukarabati zimekamilika na mradi unatoa huduma kwa wananchi.
ii.             Ukarabati na usambazaji wa maji katika kijiji cha Chase umekamilika ambapo wakazi wapatao 4,215 wananufaika na mradi huo, mradi huu umegaharimu Tshs 346,276,981.00 ambapo hadi sasa mradi umekamilika na unatoa huduma kwa wananchi.
iii.           Ukarabati na usambazaji wa maji katika kijiji cha Sori.  Mradi  huu umekamilika ambapo  wakazi wapatao 3,010 wananufaika na mradi huo, mradi huo  umegharimu  Tshs 212,187,500.00 ambapo kwa sasa unatoa huduma kwa wananchi.
iv.            Ukarabati na usambazaji wa maji katika kijiji cha Lahoda/Kisande.  Mradi huu  upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji  ambapo kukamilika kwa mradi huu kutawanufaisha  wakazi  wapatao 4,484, mradi huu ukikamilika utagharimu kiasi cha  Tshs 451,399,000.00.

       UWEKEZAJI.
        Halmashauri ya Wilaya ya chemba ina maeneo mazuri ya uwekezaji yanayotokana na uwepo wa ardhi yenye rutuba na upatikanaji wa uhakika  wa huduma ya maji, maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji katika  kilimo cha umwagiliaji  na yana vyanzo vya maji  ni pamoja na Kidoka, Kurio na Kambi ya nyasa. Hata hivyo Halmashauri inaendelea kutafuta vyanzo vingine vya maji ili kuvutia wawekezaji katika kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji na kuacha kutegemea kilimo cha msimu wa masika ambapo mvua zake hazina uhakika. Halmashauri ya Wilaya ya Chemba imetenga fedha kwa ajili ya  kujenga miundombinu ya umwagiliaji katika kijiji cha Kidoka ambapo mchakato wa maandalizi ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji  yanaendelea. Pia ujenzi wa miundombinu ya maji ikiwemo tanki, kisima cha maji na mlambo wa kunyweshea mifugo imekamilika kupitia ufadhili wa UNDP. Mradi huu umejengwa katika kijiji cha Kurio kwa  lengo la  kuwaongezea wananchi kipato kupitia kilimo cha umwagiliaji ambapo mchakato wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji bado unaendelea kupitia ufadhili wa UNDP.

        MAFANIKIO.
a)          Kukamilisha miradi ya maji ya  Chase, Waida na Sori. Miradi hii kwa sasa inatoa huduma kwa wananchi
b)          Kuendelea kukamilisha ujenzi wa Mradi wa Maji wa Lahoda/Kisande
c)           Kutekeleza sera ya Maji ya Mwaka 2002 ambapo wananchi wamehamasika kwa kuunda kamati za maji na jumuiya za watumiaji maji. Hii imesaidia wananchi kuchangia kikamilifu miradi ya maji na hivyo kuifanya kuwa endelevu.
d)          Kukamilika kwa ujenzi wa mradi wa maji kijiji cha Kurio kupitia ufadhili wa UNDP ambapo wananchi na mifugo wanapata huduma ya maji safi na salama, vilevile maji hayo yanatumika kwa ajili ya umwagiliji.

         CHANGAMOTO.
Ø  Kukosekana kwa wakandarasi mahiri wa kujenga miradi ya maji ambapo husabisha miradi kuchukua muda mrefu hadi kukamilika.
Ø  Kukosekana kwa vyanzo vya maji kwa baadhi ya maeneo yenye uhaba mkubwa wa maji. Hali hii inasababisha Halmashauri kushindwa kuwasaidia wananchi kuwapatia huduma ya maji kwa vile gharama za kutoa maji maeneo yaliyombali na vyanzo ni kubwa.
Ø  Wananchi kutoshiriki kikamilifu kuchangia asilimia 2.5 ya gharama za ujenzi wa miradi ya maji na kufanya kuwa na kiasi kidogo cha fedha.
Ø  Baadhi ya Jumuiya za watumia maji na kamati za Maji kutoshughulikia ipasavyo uendeshaji wa miradi ya Maji.
Ø  Kubadilika kwa mikondo ambayo husababisha maji kuwa na wingi wa chumvi na hatimae kutofaa kwa matumizi ya binadamu wakati kisima kimekamilika na kutoa huduma.
Ø  Kukauka kwa visima kunakosababishwa na kushuka kwa mikondo ya maji chini ya ardhi.
Ø  Wizi na ubadhirifu wa vipuri unaofanywa na watu wasiowema na maendeleo ya huduma ya Maji.

MIKAKATI.
Ø  Halmashauri hutoa matangazo ya ujenzi wa miradi kwenye vyombo mbalimbali ikiwepo PPRA ili kupata wakandarasi mahiri.
Ø  Halmashauri hupeleka ripoti kwenye vyombo husika kwa wakandarasi ambao si bora na wenye kuleta hasara.
Ø  Kuhamasisha wananchi wa vijiji visivyokuwa na kamati wala mifuko ya maji kuanzisha kamati na mifuko ya maji.
Ø  Kukarabati miundombinu ya miradi isiyotoa huduma kikamilifu, mitambo ya maji pamoja na visima virefu/kati na vifupi ili jamii ipate huduma ya maji.
Ø  Kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa uvunaji wa maji ya mvua na namna ya kujenga miundombinu ya uvunaji wa maji ya Mvua.

Jitihada zinazochukuliwa na Halmashauri ya wilaya ya Chemba katika kukabiliana na changamoto ni pamoja na:- 
a)    Kuhamasisha wananchi wa vijiji visivyokuwa na kamati wala mifuko ya maji kuanzisha kamati na mifuko ya maji.
b)   Kuwahimiza wananchi wenye mifuko ya maji kuendelea kuchangia ili miradi hiyo iwe endelevu.
c)    Kukarabati miundombinu ya miradi isiyotoa huduma kikamilifu.
d)   Kukarabati mitambo ya maji pamoja na visima virefu na vifupi ili jamii ipate huduma ya maji.
e)    Kujenga uzio na nyumba za walinzi katika maeneo ya Mitambo ya Maji.
f)     Kuhamasisha jamii itambue kuwa miradi ya maji ni mali yao.
g)   Kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa uvunaji wa maji ya mvua na namna ya kujenga miundombinu ya uvunaji wa maji ya mvua.

IDARA YA MIPANGO.
Idara ya Mipango Takwimu na Ufuatiliaji inajishughulisha na kuratibu miradi yote ya Maendeleo ikiwa ni kusimamia, ukusanyaji wa takwimu,uchambuzi na kuzisambaza kwa wadau mbalimbali wa maendeleo.Idara pia inahusika na uratibu wa uaandaji wa taarifa ya pamoja ya bajeti ya mwaka kwa halmashauri ya wilaya.

MAFANIKIO.
Idara imefanikiwa kutekeleza majukumu yafuatayo kama vile kuratibu shughuli za bajeti, kuandaa taarifa mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kila robo ya mwaka. Pia kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa miradi inayotekelezwa katika halmashauri.

 CHANGAMOTO.
Idara inakabiliwa na changamoto mbalimbali kama ifuatavyo:
i.             Ukosefu wa fedha kwa ajili ya utekelezaji na usimamizi wa miradi ya Maendeleo.
ii.             Idara haina ofisi.
iii.           Upungufu wa vitendea kazi.
iv.           Upungufu wa watumishi katika idara.
v.            Ukosefu wa gari ya idara kwa ajili ya kusimamia na kufuatilia miradi ya maendeleo.

UWEKEZAJI.
i.             Ujenzi wa stendi kuu ya magari ya abiria itachochea ukuaji wa halmashauri ya wilaya na kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa magari yatakayoingia na kutoka yatalipa ushuru.
ii.            Ujenzi wa Soko utaongeza kasi ya ukuaji wa mji wa Chemba na kuongeza shughuli mbalimbali za kiuchumi.

 IDARA YA UJENZI.
Idara ya Ujenzi inashughulika na usimamizi wa miundombinu ya barabara na majengo yaliyoko katika Idara mbalimbali za Halmashauri.

 MAFANIKIO.
i. Kuongezeka kwa mtandao wa barabara kuu za wilaya na zinazounganisha makao makuu ya wilaya, kata na vijiji.
ii.Kufunguliwa kwa barabara zinazounganisha wilaya jirani za Kondoa, Kiteto, Chamwino, Bahi, Manyoni na Singida.
iii.Kuongezeka kwa bajeti ya mfuko wa barabara kwa asilimia 49%.
Kuongezeka kwa barabara zenye tabaka la changarawe kutoka asilimia 5% hadi asilimia 20%.

CHANGAMOTO.            
 i. Bajeti ya barabara kutegemea chanzo kimoja cha fedha ambacho ni mfuko wa barabara.
ii.Ufinyu wa bajeti kulingana na mahitaji  ya mtandao wa barabara uliopo.
iii.Jamii kutoshiriki katika utunzaji wa barabara pindi zinapotengenezwa.
iv.Uharibifu wa Mazingira unaofanywa na wananchi kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu kuchangia kuharibika kwa miundombinu ya  barabara.

UWEKEZAJI.
Idara imeainisha maeneo makuu mawili ya uwekezaji kama ifuatavyo:
i.Kujenga na kufungua barabara mpya  kwenye maeneo yote ya uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo, minada na maliasili.
ii.Ujenzi wa miundombinu ya kituo cha mabasi katika  makao makuu ya wilaya karibu na eneo la barabara kuu ya Dodoma – Manyara – Arusha na barabara tarajiwa ya Tanga – Singida.


IDARA YA MIFUGO NA UVUVI.
UWEKEZAJI.
  1. Uboreshaji miundo mbinu ya mifugo katika minada 15 iliyopo  katika wilaya mfano Miundo mbinu ya maboma, mifumo ya maji,loading ramps ,mizani,  n.k
  2. Uboreshaji wa afya na mazao ya Mifugo kama vile Ujenzi na ukarabati wa Majosho, Ujenzi na ukarabati wa mabanda ya ngozi, Utoaji wa chanjo mbalimbali za Mifugo mfano Chanjo ya Mdondo kwa kuku na chambavu kwa ng'ombe.
MAFANIKIO.
i.             Idara imefanikiwa kutoa chanjo ya mdondo/kideri kwa kuku wapatao 120562 katika kipindi cha miezi 6 iliyopita.
ii.            Idara imeandika andiko kwenda LIC la kuboresha zao la ngozi katika Wilaya Chemba.

CHANGAMOTO.
i.             Upungufu wa rasilimali watu katika sekta ya mifugo.
ii.            Upungufu wa vitendea kazi hasa usafiri.
iii.           Ukosefu wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli hizi.

KITENGO CHA TEHAMA.
MAFANIKIO.
i.             Kusimamia mfumo wa ( epicor ) katika halmashauri ya Wilaya ya Chemba.
ii.            Kusimamia mfumo wa kielekroniki wa kukusanya mapato  (LGRCIS).
iii.           Kuanzisha blog ya halmashauri ya wilaya ya Chemba.
iv.           Kuweka (software) mbalimbali zinazotakiwa katika komputa za halmashauri.
v.            Kutoa ushauri wa matumizi ya vifaa vya kielekroniki.

CHANGAMOTO.
i.                    Hakuna ofisi.
ii.                  Hakuna (internet).
iii.                Hakuna (website).
iv.                 Hakuna E-mail zenye mfumo wa .go.tz au .org.tz.
MFUKO WA  TASAF.
Halmashauri ya wilaya ya Chemba iliyopo Mkoani Dodoma ni miongoni mwa Halmashauri zinazotekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na serikali kupitia TASAF Awamu ya Tatu katika vijiji  42 vilivyopo kwenye mpango.

MAFANIKIO.
Jumlaya ya kaya 5344 katika vijiji 42 vilivyopo kwenye mpango zinaendelea kunufaika na ruzuku ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini. Mafanikio ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mpaka mwezi Juni  2016  ni kuwa tangu walengwa wameanza kupokea ruzuku za fedha inaonesha kuwa wafaidika wengi (50.09%) wamenufaika kwa kuanza kuwekeza katika ufugaji wa kuku (mfano Mwapwani Mrimi Mpere wa kijiji cha Tandala amenunua kuku 8), ufugaji wa mbuzi, kilimo cha mazao mbalimbali, kununua mabati (mfano Mbula Hahaiki Soki wa kijiji cha Changamka amenunua mabati 15), ufugaji wa ng'ombe (mfano Zena Hasani Ngaso wa kijiji cha Mwaikisabe ana ngo'mbe 1), huduma za nyumbani/wasiowekeza, ufugaji wa bata, kujenga choo, kununua solar power, kununua cherehani na aliyenunua anaitwa Christina Jeremia wa Kijiji cha Mrijo chini), kununua baiskeli  na kuboresha/kujenga nyumba (mfano Juma Ramadhani Pato wa kijiji cha Madaha ameezeka nyumba anayoishi yenye vyumba viwili.
Hata hivyo ruzuku ya fedha hizi zimewasaidia sana katika suala la kujikimu kwa chakula hasa kipindi hiki kilichokuwa na upungufu mkubwa wa chakula. kwa kuongezea wamesema pia wamekuwa wakizitumia kununulia sare za shule na vifaa vingine vya wanafunzi.

Pia zimewasaidia kupata bima ya afya kwa uhakika wa matibabu kupitia mfuko wa bima ya afya ya jamii (CHF). Mpaka kufikia mwezi wa saba jumla ya kaya 3799 kati ya kaya 5251 tayari zimejiunga na CHF.
Katika kuboresha miundo mbinu ya afya programme imefanikiwa kujenga zahanati katika kijiji cha Igunga inayolenga kusogeza karibu huduma za afya na gharama ya mradi ni Tshs. 83,456,944/= ambapo fedha kutoka TASAF ambayo ni 90% ni Tshs. 74,780,944/= na mchango wa jamii ambayo ni Tshs. 8,473,000/= ambayo ni 10% mpaka kukamilika kwa mradi. Zahanati hii itapunguza adha kubwa ya wananchi wa kijiji cha Igunga kufuata huduma kijiji cha Goima au Hamai takribani kilomita 7. Mradi huu wa zahanati utahudumia wananchi wapatao 3386 katika kaya 667 zilizopo katika kijiji cha Igunga na vijiji vya jirani.

CHANGAMOTO.

i.             Mtazamo hasi wa baadhi ya wanajamii wakati wa utambuzi na uandikishaji (kwani baadhi yao wanaeneza uvumi kuwa ni mpango wa Free Mason) hivyo kufanya kazi ya ziada kuwaelimisha na kuwashawishi.
ii.            Uhitaji mkubwa kwa baadhi ya wanajamii kutaka kuingizwa kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini, kwani baadhi yao walilalamika kuwa kwa nini hawajaingizwa kwenye mpango pamoja na kuwa wao ni maskini. Hali hii ilihitaji kutoa maelezo ya ziada kuhusu bajeti na mfumo wa kompyuta unatumia vigezo maalumu katika uchambuzi wa kaya maskini.
iii.           Malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanakamati waliochaguliwa na vijiji kusaidia utekelezaji wa shughuli hizi kuwa kiasi cha posho kinachotolewa hakilingani na kazi ngumu wanafanya. Hii ilihitaji kutoa maelezo ya ziada hasa katika bajeti inavyopangwa na ndivyo malipo yanavyofanyika.
iv.           Usafiri wa kupeleka watu vijijini na kuwarudisha ni tatizo wakati wa malipo. Hivyo kulazimika kuazima au kukodi magari kutoka taasisi mbalimbali kama CCM.
v.            Malalamiko kwa baadhi ya kata hazijapewa hata kijiji kimoja kwenye Mpango wa TASAF. Hili lilifikishwa TASAF Makao Makuu na kubaliwa kuwa vitaongezewa na kutuma vijiji 42 vingine vilivyopendekezwa na wadau mbalimbali.
vi.           Walengwa kulalamikia kupungua fedha zao. Hii ilipelekea kutoa ufafanuzi kuwa wasipotimiza masharti ya elimu na afya ndipo fedha hizi hupungua.
vii.         Walengwa wanashindwa kuwekeza zaidi kutokana na changamoto ya upungufu wa chakula.
viii.        Kwa walionunua kuku baadhi ya kuku wamekufa kwa ugonjwa wa kideri baada ya kuku hao kukosa chanjo.
ix.           Kwa mradi wa ujenzi wa zahanati, wananchi kutotimiza wajibu wao wa kuchangia nguvu kazi kama mwongozo unavyosema.
x.            Asilimia ya fedha inayotengwa katika kugharamia usimamizi kutotosheleza shughuli  za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na hivyo kushindwa kufanya baadhi ya shughuli tulizojipangia ili kuboresha utekelezaji wa mpango, mfano kutoa mafunzo kwa wadau mbalimbali, kulipia gharama za matengenezo ya gari la mradi ambapo mpaka sasa tunadaiwa jumla ya Tshs.2,161,962.86/=.

MATARAJIO.
i.             Kuwekeza katika vikundi vya kaya maskini.
ii.            Kuboresha miundombinu ya elimu na afya.