Thursday, August 18, 2016

UGAWAJI WA CHAKULA KILICHOTOLEWA NA SERIKALI KWA WANANCHI WA WILAYA YA CHEMBA WALIOATHIRIKA NA UGONJWA WA SUMUKUVU.

Mkurugenzi Mtendaji (W) ya Chemba Dr.Semistatus H. Mashimba amesema, mnamo tarehe 12.08.2016 Halmashauri ya Wilaya ya Chemba ilipokea agizo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ikitaka kwenda NRFA Dodoma kupokea mahindi kiasi cha tani 60 (Gunia 684) kwa ajli ya kuwagawia wananchi walioathirika na tatizo la ugonjwa wa SUMUKUVU.
Kufuatia agizo hilo Halmashauri ya Wilaya ya Chemba ilifanya taratibu za haraka kuweza kwenda kuchukua mahindi hayo.

Magunia 229 yalisambazwa kwa wananchi waliokusudiwa katika vijiji vya Mondo, Kinkima, Itolwa, Chemka, Mlongia, Soya, Chang’ombe, Mwailanje, Mwaikisabe, na Isusumya. Magunia yaliyobaki yamehifadhiwa katika vijiji vya Chemba, Kinkima na Chemka kama tahadhari ya chakula kwa wagonjwa wengine wanaoweza kujitokeza.

Mkurugenzi Mtendaji (W) amesema, zoezi la kugawa chakula kwa wananchi walioathirika na SUMUKUVU lilifanyika kwa kushirikisha Wataalam kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji(W), Maafisa Watendaji wa Kata na vijiji wa maeneo husika na kusimamiwa kikamilifu na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Chemba.

Pia tathmini inaendelea kufanyika katika maeneo ya jirani na walikotoka wagonjwa ili kuwabaini wananchi wengine ambao wanaweza  kuwa na akiba ya chakula ambacho kimeharibika ili kukiteketeza na kuwagawia chakula kingine.Pia Halmashauri inafanya ufuatiliaji wa karibu kujua iwapo kuna wagonjwa wapya wanaojitokeza katika maeneo hayo.

Mkurugenzi Mtendaji (W) amesema, Wananchi waliopokea msaada huo wamemuomba Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Ndugu Jordan M. Rugimbana kufikisha shukrani zao za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dr. John Pombe Magufuli kwa Serikali yake ya awamu ya tano kwa msaada wa chakula waliopata.

Zifuatazo ni baadhi ya picha za matukio ya ugawaji wa chakula hicho.


1 comment: