TAARIFA
ZA IDARA/VITENGO KATIKA MAENEO YA UWEKEZAJI, MAFANIKIO NA CHANGAMOTO.
IDARA YA ELIMU SEKONDARI.
UTANGULIZI.
Idara
ya elimu sekondari imejikita zaidi kwenye taaluma katika shule za sekondari na kutoa
taarifa mbalimbali zinazohusu vyuo vilivyopo ndani ya Halmashauri. Idara
inasimamia shule za sekondari 22 za serikali na 01 ya binafsi. Kati ya shule hizi 23 kuna shule tatu (03) za
kidato cha tano ambazo ni Farkwa Sekondari, Msakwalo Sekondari na soya Sekondari.
Katika ngazi ya vyuo, idara haina chuo chochote inayosimamia katika halmashauri
yetu.
MAFANIKIO YA IDARA KWA MIAKA MITATU.
Kwa
kipindi cha miaka mitatu (2013/2014 hadi 2016/2017) idara imefanikiwa katika
shughuli zifuatazo:-
- Kuanzisha
shule za kidato cha tano. Kwa miaka mitatu sasa idara imefanikiwa
kuanzisha shule tatu za kidato cha tano michepuo ya sayansi, sanaa na
biashara. Shule hizo ni Farkwa sekondari mchepuo wa biashara kwa Tahasusi
za HGE na EGM kwa wasichana, Msakwalo sekondari mchepuo wa Sanaa kwa
Tahasusi za HGL na HGK kwa wavulana na Soya sekondari Mchepuo wa sayansi Kwa Tahasusi za PCB
na PCM wavulana. Halmashauri imefanikiwa kuwa na shule za sekondari za
Serikali kwa kila Kata isipokuwa kata ya Jangalo na Paranga ambazo zina
shule mbili kila moja. Shule zenye Daharia ni 03 tu ambazo ni Msakwalo,
Farkwa na Makorongo. Kukosekana kwa Daharia (Hostel) kunawafanya wanafunzi
watembee mwendo mrefu na kusababisha utoro kwa wanafunzi.
·
Kuongezeka ufaulu mitihani ya taifa kidato
cha Pili, Nne na Sita. Kwa muda wa miaka mitatu ufaulu wa mitihani kidato cha
pili umepanda kutoka 76% mwaka 2013, 82% mwaka 2014 na 96% mwaka 2015. Kwa
Kidato cha Nne ufaulu umepanda kutoka 48.6%
mwaka 2013 hadi 56% mwaka 2014 .
Kidato cha sita 2016 shule ya sekondari Msakwalo imefaulisha kwa asilimia 100%
na ndio matokeo ya kwanza kidato cha sita katika Halmashauri yetu.
· Ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya shule.
Idara imefanikiwa kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo:
Ø Ujenzi
wa nyumba mbili (02) za walimu shule ya sekondari Lalta na Itolwa. Pia shule
moja ya kukaa familia sita (six in one multiunit house) ambayo iko hatua ya
umaliziaji katika shule ya sekondari Mpendo.
Ø Ujenzi
wa madarasa mawili (04) shule ya
sekondari itolwa na Gwandi na Madarasa 04 shule ya sekondari Mpendo ambayo yako
hatua ya umaliziaji
Ø Ujenzi
wa matundu ya vyoo vya wanafunzi 08 na 02 ya walimu shule ya sekondari Gwandi.
Ø Ujenzi
wa maabara 01 shule ya sekondari Goima na maabara zingine 61 zikiwa kwenye
hatua mbalimbali za umaliziaji na lenta.
Ø Ufungaji
wa umeme jua kwa shule sita za sekondari ya Farkwa, Makorongo, Msakwalo,
Kwamtoro, sanzawa na Mpendo.
CHANGAMOTO.
i. Upungufu wa miundombinu na samani za shule
ikiwa ni pamoja na nyumba za walimu, maabara, maji, umeme, vyoo pamoja na
upungufu mkubwa wa viti na meza za wanafunzi pamoja na walimu.
ii.
Ukosefu wa usafiri wa idara kwa ajili ya
kufanya ufuatiliaji wa taaluma shuleni.
iii.
Ukosefu wa ofisi ya idara.
iv.
Upungufu wa rasilimali watu katika idara na
shuleni pia.
v.
Ufinyu wa bajeti ya uendeshaji wa ofisi na shule.
UWEKEZAJI.
Ujenzi
wa shule ya sekondari ya bweni kidato cha I-VI. Lengo la uhitaji wa shule 01 ya
sekondari katika makao makuu ya Chemba ni kuweza kuwa na shule 01 ya Bweni
kidato cha kwanza hadi Sita iliyo kamilika katika Miundombinu yote. Fursa
zinazoiwezesha shule hii ni pamoja na:
i)
Kuwepo kwa eneo lililopimwa tayari kwa ajili
ya ujenzi wa shule hiyo.
ii)
Makao makuu ya wilaya kutokuwa na shule ya
sekondari kwani shule ya kata ipo umbali wa kilomita 10 toka makao makuu ya
wilaya. Umbali huu unasababisha wanafunzi wa wakazi wa Chemba kutoifikia shule
hiyo kwa urahisi.
iii)
Kuwa na shule 01 ya mfano ya bweni
iliyokamilika kwa miundombinu kuanzia kidato cha Kwanza hadi cha Sita.
UMALIZIAJI
WA UJENZI WA DAHARIA KWA KILA SHULE YA SEKONDARI.
Kati
ya shule 22 za sekondari za Serikali wilaya ya Chemba ni shule 03 tu ndizo
zenye Daharia (Hosteli) ambazo ni Msakwalo, Farkwa na Makorongo. Lengo la
ujenzi wa Daharia kwa kila shule ya sekondari ni kuboresha mazingira ya
kujifunzia na kufundishia.
Jumla
ya Daharia 38 zinatakiwa zijengwe kwa shule 19, kila shule inatakiwa na Daharia
02.
Lengo
la ujenzi wa Daharia (Hostel) ni:
i)
Kuondoa utoro wa rejareja na wa kudumu kwa
wanafunzi, hii ni kutokana na shule nyingi za sekondari kuwa mbali na maeneo
wanakoishi jamii. Imebainika kwamba wanafunzi wanaotoka umbali wa kilomita 10
na zaidi wameonekana kuwa watoro shuleni.
ii) Kuinua taaluma kwani wanafunzi wanapo kuwa
wanaishi shuleni wanakuwa na muda mwingi wa kujisomea na kuondokana na shughuli
za kijamii zinazoathiri ujifunzaji kwa wanafunzi.
iii) Kupunguza tatizo la Wanafunzi wa kike kupata
ujauzito.Imethibitika kwamba wanafunzi wa kike wanapata vishawishi wawapo
uraiani kuliko shule za Bweni.
iv) Kuinua taaluma kwani wanafunzi wanapo kuwa
wanaishi shuleni wanakuwa na muda mwingi wa kujisomea na kuondokana na shughuli
za kijamii zinazoathiri ujifunzaji kwa wanafunzi.
v) Kupunguza tatizo la Wanafunzi wa kike kupata
ujauzito.Imethibitika kwamba wanafunzi wa kike wanapata vishawishi wawapo
uraiani kuliko shule za Bweni.
IDARA YA ARDHI NA MALIASILI.
UWEKEZAJI.
Idara
ya Ardhi na Maliasili imebainisha maeneo yafuatayo kwa ajili ya uwekezaji
katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba.
i.
Uwekezaji wa viwanda vidogovidogo na
vikubwa, shule za awali kwa ajili ya kuvutia wawakezaji mbali mbali na kusogeza
huduma karibu na jamii.
ii.
Ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kupitia
Shirika la nyumba la Taifa (NHC) ili kuweza kukidhi matakwa ya watumishi kwa
kupata makazi katika makao makuu ya Wilaya ya Chemba. Pia maeneo ya sokoni,
stendi ya mabasi, hospitali inatakiwa viwanja vyake kuendelezwa kwa haraka
zaidi ili wananchi waweze kupata huduma muhimu.
iii.
Maeneo mengine ni benki, shule za Msingi na
sekondari, vyuo, Ufugaji wa nyuki naTaasisi zingine zinazo jishughulisha na
shughuli za maendeleo.
MAFANIKIO.
Katika
mwaka wa fedha 2015/2016 Idara ya Ardhi na Maliasili imefanikiwa katika mambo yafuatayo;
ARDHI.
Kupima viwanja vya matumizi mbalimbali
vipatavyo 539 kitalu A na 596 kitalu D katika makao makuu ya Wilaya ya Chemba.
Pia tulishapima viwanja 654 kitalu B na watu wanaendelea kujenga majengo
yanayokidhi mahitaji ya ujenzi bora na wa kisasa.
NYUKI.
i.
Kuwezesha Halmashauri kuwa na mpango mkakati
wa kuendeleza ufugaji nyuki kiwilaya na sheria ndogo ndogo za Wilaya kuhusu
kuendeleza raslimali ya nyuki.
ii.
Kwa kushirikiana na WVI Tanzania, Farkwa ADP
Kuwezesha uanzishwaji wa manzuki ya mfano na mafunzo shule ya sekondari Farkwa
yenye jumla ya mizinga ya kisasa 200.
MISITU.
i.
Kudhibiti uvunaji na
usafirishaji haramu wa mazao ya misitu. Doria zilifanyika katika maeneo ya Kata
za Kwamtoro na Farkwa, kuimarisha ukaguzi katika Mageti ya Babayu, Kinyamsindo,
Mrijo, Kidoka na Tandala. Kazi hii imefanyika kwa ushirikiano na TFS.
ii.
Kuendelea na zoezi la
usimamizi wa ukusanyaji wa mbao za madawati kwa ajili ya shule za Msingi na
Sekondari, Kazi inaendelea na Mafanikio ni makubwa
hadi sasa.
WANYAMAPORI.
Ufuatiliaji
wa Taarifa za wanyamapori wakali na wakubwa , Kazi hii imefanyika kwa
ushirikiano wa Pori la akiba Swagaswaga , Mkungunero na Polisi Chemba katika
maeneo ya vijiji vya Tandala, Mtakuja, Igunga, Mialo na Kwamtoro.
CHANGAMOTO.
i.
Wananchi wenyeji hawabadiliki kutokana na mji
unavyotakiwa kwa kujenga majengo bora, kuhamisha mifugo n.k.
ii.
Dhana ya kugawana viwanja halmashauri na
wananchi imesababisha misuguano na wananchi wenye maeneo yao.
iii.
Kutokuwepo kwa fedha za kupima maeneo yaliyobakia.
iv.
Matumizi ya madawa ya kilimo ambayo
yanasababisha vifo vya nyuki.
v.
Uchomaji
moto mapori ambao unaunguza miti muhimu kwa utoaji wa asali na mizinga.
vi.
Ufyekaji
wa misitu unaofanywa na wakulima wakati wa kuandaa mashamba mapya ya kilimo.
MIKAKATI.
i. Kuendelea na utoaji wa elimu kwa wananchi
kwa kushirikiana na idara zenye ushawishi mkubwa kama vile maendeleo ya jamii.
ii.
Kuandika andiko la kuomba mkopo ili kulipa
fidia na kupima maeneo ya block C, E, na F ili kuweza kudhibiti uendelezaji
holela wa viwanja.
iii.
Kutoa elimu ya utunzaji wa Mazingira kwa
wananchi ya kupanda miti kwenye maeneo yao pamoja na kulinda hifadhi ya
milima inayozunguka Wilaya ili iweze kuwa na mandhari inayovutia na kuleta
hewa safi kwa kushirikiana na Idara ya Mazingira.
iv.
Uwanzishwaji wa mashamba manne ya
uendelezaji ufugaji nyuki kwa kushirikiana na Wakala wa huduma za Misitu
Tanzania (Tanzania Forest Service (TFS).
IDARA YA ELIMU MSINGI.
UWEKEZAJI.
- Kuanzisha/kujenga
shule ya ufundi (VETA) katika kijiji cha kambi ya nyasa.
- Kuanzisha/kujenga
shule ya Kiingereza (Medium school darasa la Awali – Kidato cha nne)
katika kijiji cha Kambi ya Nyasa.
- Kuanzisha/kujenga
shule maalum ya watoto wasioona na viziwi (Darasa la Awali - Darasa la saba.
MAFANIKIO.
i.
Kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu wa mtihani
wa darasa la saba kutoka asilimia 30 hadi 47.
ii. Waratibu
Elimu Kata kuwezeshwa usafiri wa Pikipiki pamoja na rukuzu kwa ufadhili wa
mpango wa Equip – Tanzania inayorahisisha ukaguzi wa shule kwa lengo la kuinua
taaluma shuleni.
iii. Kuongezeka
kwa kiwango cha uandikishaji kwa kuanzishwa madarasa 70 ya utayari chini ya
Mpango wa Equip – Tanzania.
iv. Walimu
Wakuu na Waratibu Elimu Kata kupata mafunzo ya uongozi chini ya mpango wa Equip
– Tanzania.
v. Walimu
kupatiwa mafunzo kazini ambayo yamesaidia kupunguza idadi ya wanafunzi wasiojua
KKK.
vi. Kamati
za shule zote 103 kujengewa uwezo wa kusimamia shule.
CHANGAMOTO.
i. Ukosefu
wa usafiri (gari la Idara ya elimu).
ii. Upungufu
mkubwa wa miundombinu na samani mfano madarasa na nyumba za walimu, meza, viti
na kabati.
iii. Kuwepo
kwa miundo mbinu ya shule isiyokamilika mfano katika nyumba za walimu na
madarasa.
iv. Upungufu
wa vitendea kazi kwa ajili ya mifumo ya taarifa kama vile internet, komputa,
printa na mashine ya kudurufu.
v. Maeneo
ya shule kutopimwa na kukosa Hati miliki.
vi. Uchakavu
wa miundo mbinu ya shule.
vii. Ukosefu
wa vyumba maalum (Strong room) kwa ajili ya kuhifadhia mtihani.
IDARA YA KILIMO, UMWAGILIAJI NA
USHIRIKA.
UWEKEZAJI.
i.
Kujenga masoko ya mazao kwenye maeneo ya
kata ambayo uzalishaji wa mazao ni mkubwa, mfano Mrijo, Soya, Kidoka, Jangalo
n.k.
ii.
Kuanzisha/kujenga skimu za umwagiliaji
katika maeneo yenye fursa hiyo(potential areas)
Mfano; Kidoka, Paranga na
Jogolo.
CHANGAMOTO.
i.
Bei za mazao kubadilika mara kwa mara.
ii.
Upungufu wa raslimali watu.
iii.
Kutokuwa na usafiri.
iv.
Kutopata fedha za miradi kwa wakati.
MAFANIKIO.
i. Tumeendelea kutoa huduma za ugani kwa
kutumia mbinu mbalimbali mfano kuanzisha mashamba darasa,mashamba ya mfano n.k
ii. Tumeendelea kusimamia miradi ya idara ya
kilimo katika wilaya yetu, kwa mfano; miradi ya ujenzi wa maghala ya kuhifadhia
mazao na ujenzi wa mashine za kukamulia alizeti.
IDARA YA MAENDELEO YA JAMII.
MAFANIKIO.
i.
Idara imeweza kuhamasisha uanzishaji na
kusajili jumla ya vikundi 460 vya uzalishaji mali vya kiuchumi na kijamii.
ii.
Jumla ya kaya 85 zimepata mafunzo ya
ujasiliamali, ufugaji nyuki wa kisasa pamoja na mradi wa ufugaji nyuki.
iii.
Idara imefanikiwa kuwezesha kaya masikini
5,344 kupitia mpango wa TASAF III.
iv.
Tumefanikiwa kutoa mikopo yenye riba nafuu
kwa vikundi vya uzalishaji mali vya wanawake
12 na vya vijana 9.
v.
Tumefanikiwa kuwalipia ada na michango
muhimu watoto 143 waishio katika mazingira hatarishi waliopo shule za sekondari
na vyuo.
vi.
Idara imefanikiwa kuunda kamati za kusaidia
watoto waishio katika mazingira hatarishi katika vijiji 10 kwa kushirikiana na
shirika lisilo la kiserikali la CCT pamoja TUWALEE.
CHANGAMOTO.
i.
Ukosefu wa fedha za kutosha za kuwezesha
vikundi vya wanawake na vijana.
ii.
Uhaba wa rasilimali watu katika idara.
iii.
Uhaba wa rasilimali fedha zinazotolewa
ambazo ni ruzuku katoka serikali kuu.
iv.
Ukosefu wa vitendea kazi katika ofisi kama
kompyuta na printa.
MATARAJIO YA IDARA.
i.
Kutoa mafunzo endelevu ya uingizwaji masuala
ya jinsia katika mipango na bajeti ngazi zote.
ii.
Kuwa na mfuko endelevu wa utoaji wa elimu
jinsia.
iii.
Kutoa elimu ya kuweka na kukopa kwa vikundi
vya wanawake na vijana.
MFUKO WA AFYA YA JAMII (CHF).
UWEKEZAJI.
i.Kutafuta wadau mbalimbali kulipia
kaya maskini kama; wafanyabiashara, viongozi mbalimbali ili kuongeza idadi ya
kaya zisizojiweza kunufaika na huduma hii.
ii.Kuongeza uhamasishaji kwa kutumia
mbinu mbalimbali.
CHANGAMOTO.
i.Upungufu wa watumishi wa afya katika
sehemu za kutolea huduma.
ii.Watoa huduma wengi kutojua jinsi ya
kuwasilisha madai.
iii.Kutokuwa na fedha za kutosha kwa
ajili ya kufanya uhamasishaji.
MAFANIKIO.
i.
Tumefanikiwa kuandikisha kaya 10,401 kati
39,285 kwa kaya lengwa kwa wilaya ya chemba,na kufikia asilimia 26.48% ya
uandikishaji.
ii.
Tumefanikiwa kufanya uhamasishaji juu ya
malengo, umhimu, mfumo na faida za CHF kwa maeneo mengi ya wilaya ya Chemba.
IDARA YA MAJI
Hali
ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Halmashauri ya wilaya ya
Chemba ni kuwa wakazi wapatao 73,231 kati ya 235,711 wanapata huduma ya maji
safi na salama sawa na asilimia 31 ya wakazi wote. Idara ya maji Wilaya ya
Chemba inaendelea na jitihada za kutafuta vyanzo vingine vya maji ili wananchi
ambao hawajafikiwa na huduma ya maji waweze kupata maji safi na salama ndani ya
mita 400 kama sera ya maji ya mwaka 2002 inavyoelekeza.
UBORESHAJI WA HUDUMA YA MAJI.
Halmashauri ya Wilaya ya Chemba imekarabati na
inaendelea na ukarabati wa miradi
ya maji yenye kuleta matokeo ya haraka (Quick wins) katika vijiji vya waida,
Chase, sori na Lahoda/Kisande ambapo mchakato wake umefanyika na Halmashauri ya
Wilaya ya Chemba.
Utekelezaji wa Miradi ya maji ni kama ifuatavyo;
i.
Ukarabati
na usambazaji wa maji katika kijiji cha
waida umekamilika ambapo wakazi
wapatao 2,622 wananufaika na mradi huo,
mradi huu umegharimu Tshs. 168,950,000.00 ambapo kazi za ukarabati zimekamilika
na mradi unatoa huduma kwa wananchi.
ii.
Ukarabati na usambazaji wa maji katika kijiji
cha Chase umekamilika ambapo wakazi wapatao 4,215 wananufaika na mradi huo,
mradi huu umegaharimu Tshs 346,276,981.00 ambapo hadi sasa mradi umekamilika na
unatoa huduma kwa wananchi.
iii.
Ukarabati
na usambazaji wa maji katika kijiji cha Sori.
Mradi huu umekamilika ambapo wakazi wapatao 3,010 wananufaika na mradi
huo, mradi huo umegharimu Tshs 212,187,500.00 ambapo kwa sasa unatoa
huduma kwa wananchi.
iv.
Ukarabati na usambazaji wa maji katika kijiji
cha Lahoda/Kisande. Mradi huu upo katika hatua za mwisho za
ukamilishaji ambapo kukamilika kwa mradi
huu kutawanufaisha wakazi wapatao 4,484, mradi huu ukikamilika
utagharimu kiasi cha Tshs
451,399,000.00.
UWEKEZAJI.
Halmashauri
ya Wilaya ya chemba ina maeneo mazuri ya uwekezaji yanayotokana na uwepo wa
ardhi yenye rutuba na upatikanaji wa uhakika
wa huduma ya maji, maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji
katika kilimo cha umwagiliaji na yana vyanzo vya maji ni pamoja na Kidoka, Kurio na Kambi ya nyasa.
Hata hivyo Halmashauri inaendelea kutafuta vyanzo vingine vya maji ili kuvutia
wawekezaji katika kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji na kuacha kutegemea
kilimo cha msimu wa masika ambapo mvua zake hazina uhakika. Halmashauri ya
Wilaya ya Chemba imetenga fedha kwa ajili ya
kujenga miundombinu ya umwagiliaji katika kijiji cha Kidoka ambapo
mchakato wa maandalizi ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji yanaendelea. Pia ujenzi wa miundombinu ya
maji ikiwemo tanki, kisima cha maji na mlambo wa kunyweshea mifugo imekamilika
kupitia ufadhili wa UNDP. Mradi huu umejengwa katika kijiji cha Kurio kwa lengo la
kuwaongezea wananchi kipato kupitia kilimo cha umwagiliaji ambapo
mchakato wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji bado unaendelea kupitia
ufadhili wa UNDP.
MAFANIKIO.
a)
Kukamilisha miradi ya maji ya Chase, Waida na Sori. Miradi hii kwa sasa
inatoa huduma kwa wananchi
b)
Kuendelea kukamilisha ujenzi wa Mradi wa
Maji wa Lahoda/Kisande
c)
Kutekeleza sera ya Maji ya Mwaka 2002
ambapo wananchi wamehamasika kwa kuunda kamati za maji na jumuiya za watumiaji
maji. Hii imesaidia wananchi kuchangia kikamilifu miradi ya maji na hivyo
kuifanya kuwa endelevu.
d)
Kukamilika kwa ujenzi wa mradi wa maji
kijiji cha Kurio kupitia ufadhili wa UNDP ambapo wananchi na mifugo wanapata
huduma ya maji safi na salama, vilevile maji hayo yanatumika kwa ajili ya
umwagiliji.
Ø Kukosekana
kwa wakandarasi mahiri wa kujenga miradi ya maji ambapo husabisha miradi
kuchukua muda mrefu hadi kukamilika.
Ø Kukosekana
kwa vyanzo vya maji kwa baadhi ya maeneo yenye uhaba mkubwa wa maji. Hali hii
inasababisha Halmashauri kushindwa kuwasaidia wananchi kuwapatia huduma ya maji
kwa vile gharama za kutoa maji maeneo yaliyombali na vyanzo ni kubwa.
Ø Wananchi
kutoshiriki kikamilifu kuchangia asilimia 2.5 ya gharama za ujenzi wa miradi ya
maji na kufanya kuwa na kiasi kidogo cha fedha.
Ø Baadhi
ya Jumuiya za watumia maji na kamati za Maji kutoshughulikia ipasavyo
uendeshaji wa miradi ya Maji.
Ø Kubadilika
kwa mikondo ambayo husababisha maji kuwa na wingi wa chumvi na hatimae kutofaa
kwa matumizi ya binadamu wakati kisima kimekamilika na kutoa huduma.
Ø Kukauka
kwa visima kunakosababishwa na kushuka kwa mikondo ya maji chini ya ardhi.
Ø Wizi
na ubadhirifu wa vipuri unaofanywa na watu wasiowema na maendeleo ya huduma ya
Maji.
MIKAKATI.
Ø Halmashauri
hutoa matangazo ya ujenzi wa miradi kwenye vyombo mbalimbali ikiwepo PPRA ili
kupata wakandarasi mahiri.
Ø Halmashauri
hupeleka ripoti kwenye vyombo husika kwa wakandarasi ambao si bora na wenye
kuleta hasara.
Ø Kuhamasisha
wananchi wa vijiji visivyokuwa na kamati wala mifuko ya maji kuanzisha kamati
na mifuko ya maji.
Ø Kukarabati
miundombinu ya miradi isiyotoa huduma kikamilifu, mitambo ya maji pamoja na
visima virefu/kati na vifupi ili jamii ipate huduma ya maji.
Ø Kuhamasisha
jamii juu ya umuhimu wa uvunaji wa maji ya mvua na namna ya kujenga miundombinu
ya uvunaji wa maji ya Mvua.
Jitihada
zinazochukuliwa na Halmashauri ya wilaya ya Chemba katika kukabiliana na changamoto
ni pamoja na:-
a) Kuhamasisha
wananchi wa vijiji visivyokuwa na kamati wala mifuko ya maji kuanzisha kamati
na mifuko ya maji.
b) Kuwahimiza
wananchi wenye mifuko ya maji kuendelea kuchangia ili miradi hiyo iwe endelevu.
c) Kukarabati
miundombinu ya miradi isiyotoa huduma kikamilifu.
d) Kukarabati
mitambo ya maji pamoja na visima virefu na vifupi ili jamii ipate huduma ya
maji.
e) Kujenga
uzio na nyumba za walinzi katika maeneo ya Mitambo ya Maji.
f) Kuhamasisha
jamii itambue kuwa miradi ya maji ni mali yao.
g) Kuhamasisha
jamii juu ya umuhimu wa uvunaji wa maji ya mvua na namna ya kujenga miundombinu
ya uvunaji wa maji ya mvua.
IDARA
YA MIPANGO.
Idara
ya Mipango Takwimu na Ufuatiliaji inajishughulisha na kuratibu miradi yote ya
Maendeleo ikiwa ni kusimamia, ukusanyaji wa takwimu,uchambuzi na kuzisambaza
kwa wadau mbalimbali wa maendeleo.Idara pia inahusika na uratibu wa uaandaji wa
taarifa ya pamoja ya bajeti ya mwaka kwa halmashauri ya wilaya.
MAFANIKIO.
Idara
imefanikiwa kutekeleza majukumu yafuatayo kama vile kuratibu shughuli za
bajeti, kuandaa taarifa mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa
kila robo ya mwaka. Pia kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa miradi
inayotekelezwa katika halmashauri.
CHANGAMOTO.
Idara
inakabiliwa na changamoto mbalimbali kama ifuatavyo:
i.
Ukosefu wa fedha kwa ajili ya utekelezaji na
usimamizi wa miradi ya Maendeleo.
ii.
Idara
haina ofisi.
iii.
Upungufu wa vitendea kazi.
iv.
Upungufu wa watumishi katika idara.
v.
Ukosefu wa gari ya idara kwa ajili ya kusimamia
na kufuatilia miradi ya maendeleo.
UWEKEZAJI.
i.
Ujenzi wa stendi kuu ya magari ya abiria
itachochea ukuaji wa halmashauri ya wilaya na kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa
magari yatakayoingia na kutoka yatalipa ushuru.
ii.
Ujenzi wa Soko utaongeza kasi ya ukuaji wa
mji wa Chemba na kuongeza shughuli mbalimbali za kiuchumi.
IDARA YA UJENZI.
Idara ya Ujenzi inashughulika na usimamizi wa miundombinu
ya barabara na majengo yaliyoko katika Idara mbalimbali za Halmashauri.
MAFANIKIO.
i. Kuongezeka kwa mtandao wa barabara kuu za wilaya na
zinazounganisha makao makuu ya wilaya, kata na vijiji.
ii.Kufunguliwa kwa barabara zinazounganisha wilaya jirani
za Kondoa, Kiteto, Chamwino, Bahi, Manyoni na Singida.
iii.Kuongezeka kwa bajeti ya mfuko wa barabara kwa
asilimia 49%.
Kuongezeka kwa barabara zenye tabaka la changarawe kutoka
asilimia 5% hadi asilimia 20%.
CHANGAMOTO.
i. Bajeti ya
barabara kutegemea chanzo kimoja cha fedha ambacho ni mfuko wa barabara.
ii.Ufinyu wa bajeti kulingana na mahitaji ya mtandao wa barabara uliopo.
iii.Jamii kutoshiriki katika utunzaji wa barabara pindi
zinapotengenezwa.
iv.Uharibifu wa Mazingira unaofanywa na wananchi kutokana
na shughuli mbalimbali za kibinadamu kuchangia kuharibika kwa miundombinu
ya barabara.
UWEKEZAJI.
Idara imeainisha maeneo makuu mawili ya uwekezaji kama
ifuatavyo:
i.Kujenga na kufungua barabara mpya kwenye maeneo yote ya uzalishaji wa mazao ya
kilimo, mifugo, minada na maliasili.
ii.Ujenzi wa miundombinu ya kituo cha mabasi katika makao makuu ya wilaya karibu na eneo la
barabara kuu ya Dodoma – Manyara – Arusha na barabara tarajiwa ya Tanga –
Singida.
IDARA YA MIFUGO NA UVUVI.
UWEKEZAJI.
- Uboreshaji
miundo mbinu ya mifugo katika minada 15 iliyopo katika wilaya mfano Miundo mbinu ya maboma,
mifumo ya maji,loading ramps ,mizani,
n.k
- Uboreshaji
wa afya na mazao ya Mifugo kama vile Ujenzi na ukarabati wa Majosho, Ujenzi
na ukarabati wa mabanda ya ngozi, Utoaji wa chanjo mbalimbali za Mifugo
mfano Chanjo ya Mdondo kwa kuku na chambavu kwa ng'ombe.
MAFANIKIO.
i.
Idara imefanikiwa kutoa chanjo ya
mdondo/kideri kwa kuku wapatao 120562 katika kipindi cha miezi 6 iliyopita.
ii.
Idara imeandika andiko kwenda LIC la
kuboresha zao la ngozi katika Wilaya Chemba.
CHANGAMOTO.
i.
Upungufu wa rasilimali watu katika sekta ya
mifugo.
ii.
Upungufu wa vitendea kazi hasa usafiri.
iii.
Ukosefu wa rasilimali fedha kwa ajili ya
utekelezaji wa shughuli hizi.
KITENGO CHA TEHAMA.
MAFANIKIO.
i.
Kusimamia mfumo wa ( epicor ) katika
halmashauri ya Wilaya ya Chemba.
ii.
Kusimamia mfumo wa kielekroniki wa kukusanya
mapato (LGRCIS).
iii.
Kuanzisha blog ya halmashauri ya wilaya ya
Chemba.
iv.
Kuweka (software) mbalimbali zinazotakiwa
katika komputa za halmashauri.
v.
Kutoa ushauri wa matumizi ya vifaa vya
kielekroniki.
CHANGAMOTO.
i.
Hakuna ofisi.
ii.
Hakuna (internet).
iii.
Hakuna (website).
MFUKO WA
TASAF.
Halmashauri ya wilaya ya Chemba iliyopo Mkoani Dodoma ni
miongoni mwa Halmashauri zinazotekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa
na serikali kupitia TASAF Awamu ya Tatu katika vijiji 42 vilivyopo kwenye mpango.
MAFANIKIO.
Jumlaya
ya kaya 5344 katika vijiji 42 vilivyopo kwenye mpango zinaendelea kunufaika na
ruzuku ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini. Mafanikio ya Mpango wa Kunusuru Kaya
Maskini mpaka mwezi Juni 2016 ni kuwa tangu walengwa wameanza kupokea
ruzuku za fedha inaonesha kuwa wafaidika wengi (50.09%) wamenufaika kwa kuanza
kuwekeza katika ufugaji wa kuku (mfano
Mwapwani Mrimi Mpere wa kijiji cha Tandala amenunua kuku 8), ufugaji wa mbuzi,
kilimo cha mazao mbalimbali, kununua mabati (mfano Mbula Hahaiki Soki wa kijiji
cha Changamka amenunua mabati 15), ufugaji wa ng'ombe (mfano Zena Hasani Ngaso
wa kijiji cha Mwaikisabe ana ngo'mbe 1), huduma za nyumbani/wasiowekeza,
ufugaji wa bata, kujenga choo, kununua solar power, kununua cherehani na aliyenunua
anaitwa Christina Jeremia wa Kijiji cha Mrijo chini), kununua baiskeli na kuboresha/kujenga nyumba (mfano Juma
Ramadhani Pato wa kijiji cha Madaha ameezeka nyumba anayoishi yenye vyumba
viwili.
Hata
hivyo ruzuku ya fedha hizi zimewasaidia sana katika suala la kujikimu kwa
chakula hasa kipindi hiki kilichokuwa na upungufu mkubwa wa chakula. kwa
kuongezea wamesema pia wamekuwa wakizitumia kununulia sare za shule na vifaa
vingine vya wanafunzi.
Pia
zimewasaidia kupata bima ya afya kwa uhakika wa matibabu kupitia mfuko wa bima
ya afya ya jamii (CHF). Mpaka kufikia mwezi wa saba jumla ya kaya 3799 kati ya
kaya 5251 tayari zimejiunga na CHF.
Katika
kuboresha miundo mbinu ya afya programme imefanikiwa kujenga zahanati katika
kijiji cha Igunga inayolenga kusogeza karibu huduma za afya na gharama ya mradi
ni Tshs. 83,456,944/= ambapo fedha
kutoka TASAF ambayo ni 90% ni Tshs.
74,780,944/= na mchango wa jamii ambayo ni Tshs. 8,473,000/= ambayo ni 10% mpaka kukamilika kwa mradi.
Zahanati hii itapunguza adha kubwa ya wananchi wa kijiji cha Igunga kufuata
huduma kijiji cha Goima au Hamai takribani kilomita 7. Mradi huu wa zahanati utahudumia wananchi wapatao
3386 katika kaya 667 zilizopo katika kijiji cha Igunga na vijiji vya jirani.
CHANGAMOTO.
i.
Mtazamo hasi wa baadhi ya wanajamii wakati
wa utambuzi na uandikishaji (kwani baadhi yao wanaeneza uvumi kuwa ni mpango wa
Free Mason) hivyo kufanya kazi ya ziada kuwaelimisha na kuwashawishi.
ii.
Uhitaji mkubwa kwa baadhi ya wanajamii
kutaka kuingizwa kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini, kwani baadhi yao
walilalamika kuwa kwa nini hawajaingizwa kwenye mpango pamoja na kuwa wao ni
maskini. Hali hii ilihitaji kutoa maelezo ya ziada kuhusu bajeti na mfumo wa
kompyuta unatumia vigezo maalumu katika uchambuzi wa kaya maskini.
iii.
Malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanakamati
waliochaguliwa na vijiji kusaidia utekelezaji wa shughuli hizi kuwa kiasi cha
posho kinachotolewa hakilingani na kazi ngumu wanafanya. Hii ilihitaji kutoa
maelezo ya ziada hasa katika bajeti inavyopangwa na ndivyo malipo
yanavyofanyika.
iv.
Usafiri wa kupeleka watu vijijini na
kuwarudisha ni tatizo wakati wa malipo. Hivyo kulazimika kuazima au kukodi
magari kutoka taasisi mbalimbali kama CCM.
v.
Malalamiko
kwa baadhi ya kata hazijapewa hata kijiji kimoja kwenye Mpango wa TASAF. Hili
lilifikishwa TASAF Makao Makuu na kubaliwa kuwa vitaongezewa na kutuma vijiji
42 vingine vilivyopendekezwa na wadau mbalimbali.
vi.
Walengwa
kulalamikia kupungua fedha zao. Hii ilipelekea kutoa ufafanuzi kuwa
wasipotimiza masharti ya elimu na afya ndipo fedha hizi hupungua.
vii.
Walengwa
wanashindwa kuwekeza zaidi kutokana na changamoto ya upungufu wa chakula.
viii.
Kwa
walionunua kuku baadhi ya kuku wamekufa kwa ugonjwa wa kideri baada ya kuku hao
kukosa chanjo.
ix.
Kwa mradi wa ujenzi wa zahanati, wananchi
kutotimiza wajibu wao wa kuchangia nguvu kazi kama mwongozo unavyosema.
x.
Asilimia
ya fedha inayotengwa katika kugharamia usimamizi kutotosheleza shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na hivyo
kushindwa kufanya baadhi ya shughuli tulizojipangia ili kuboresha utekelezaji
wa mpango, mfano kutoa mafunzo kwa wadau mbalimbali, kulipia gharama za
matengenezo ya gari la mradi ambapo mpaka sasa tunadaiwa jumla ya Tshs.2,161,962.86/=.
MATARAJIO.
i.
Kuwekeza katika vikundi vya kaya maskini.
ii.
Kuboresha miundombinu ya elimu na afya.